Wahenga walisema kuwa usiku wa dhiki huwa mrefu kuliko kawaida ,
msemo huu unaonekana kuwahusu zaidi wazee wa Green City aka Mbeya City
ambao hii leo wameshuhudia timu yao ikipoteza mchezo wake wa tatu
mfululizo katika muendelezo wa ligi kuu ya Tanzania bara akak VPL
.
Mbeya City ambao hii leo walikuwa wakimalizia kiporo kilicholala siku
ya jumapili baada ya mchezo wao kuahirishwa walifungwa 2-1 na maafande
wa Mgambo Shooting katika mchezo uliopigwa kwneye uwanja wa Ccm
Mkwakwani huko Tanga .
Mbeya City ambao msimu huu wameuanza vibaya baada ya kufanya vizuri
na kuwashangaza wengi msimu uliopita waliuanza mchezo kwa kasi ya chini
hali iliyowafanya kufungwa bao la kwanza mapema kwenye kipindi cha
kwanza mfungaji akiwa Malime Busungu aliyefunga kwa mkwaju wa penati
baada ya beki wa Mbeya City Yohana Morris kufanya madhambi kwenye eneo
la hatari .
Zikiwa zimepita dakika chache baada ya kipa David Burhani kuokota
mpira wavuni kwake , alijikuta akirejea kitendo kama hicho baada ya
kushindwa kuzia shuti la kiungo Ali Nassor Iddi ambaye alimalizia kazi
nzuri iliyofanywa na mfungaji wa bao la kwanza Malime Busungu .
Kipindi cha kwanza kiliisha huku Mgambo wakizidi kulisakama lango la
Mbeya City na kama isingekuwa uzembe wa washambuliaji Mgambo wangeweza
kumaliza dakika 45 za kwanza wakiwa na mabao zaidi .
Katika kipindi cha pili Mbeya City walifanya mabadiliko ya kuongeza
nguvu safu ya ushambuliaji kwa kuwaingiza Saad Kipanga na Hamad Hamza
Kibopile .
Mbadiliko haya yalileta uhai kwani winga Deus Kaseke aliifunia Mbeya
City bao lao pekee katika mchezo huo , bao ambalo hata hivyo halikutosha
kuwazuia Mgambo wasiondoke na ushindi wao wa tatu katika msimu huu .
Ushindi huu unawafanya Mgambo kuruka mpaka kwenye nafasi ya sita
wakiwa wamejikusanyia pointi tisa zinazotokana na mechi tatu
walizoshinda huku wakiwa wamepoteza michezo mitatu pia .
Kwa upande wa Mbeya City hali imezidi kuwa mbaya kwani wanajikuta
wanapoteza mchezo wa tatu mfululizo hali ambayo itazidi kumpa ‘stress’
kocha wao Juma Mwambusi .
Blogger Comment
Facebook Comment