Waziri mkuu wa Italia Matteo Renzi
ametoa wito wa kufanyika kikao cha dharura cha viongozi wa umoja wa
ulaya kujadili swala la wahamiaji wanaoangamia kwenye bahari ya
Meditarenean wakijaribu kuingia ulaya. Inafuatia ajali ya hivi punde
ambao karibu watu 700 wanahofiwa kufa maji baada ya boti kuzama baharini
kaskazini mwa Libya, kilomita 200 kutoka kisiwa cha Lampedusa, nchini
Italia.
Manusura 28 wa janga la hivi punde kwenye bahari ya
Meditaranean walitarajiwa kufikishwa kisiwani Sicily alfajiri ya
Jumatatu. Hadi kufikia usiku, ni miili 24 iliyokuwa imeopolewa, na
maafisa wa usalama kwenye pwani ya Italia, wakaipeleka kisiwani Malta.
Ni
vigumu kuhakikisha idadi ya watu walioanza safari kwenye boti hiyo
kutoka pwani ya Libya. Lakini walionusurika wanasema walikuwa kati ya
watu 500 na 700 kabla ya kupinduka kilomita mia mbili kutoka Lampedusa,
kwenye maji ya Libya.
Ikiwa idadi hiyo itathibitishwa basi hii
itakuwa ndio ajali mbaya zaidi kati ya nyingi ambazo zimekuwa zikitokea
karibuni kwenye bahari ya mediteranean, huku watu wakifanya safari za
hatari kutafuta maisha bora ulaya.
Waziri mkuu wa Italia Matteo
Renzi amesema zaidi ya mawakala 900 wa kusafirisha watu wamekamatwa.
Alisema suluhu la tatizo la wahamiaji si kutafuta manusura baharini,
bali kuwakabili mawakala hao wa kusafirisha watu, akiwaita
wafanyabiashara wa watumwa wa leo. Ametaka kikao cha umoja wa ulaya
ndani ya wiki moja kujadili tatizo hili kubwa.
Papa Francis kwenye
misa ya Jumapili alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua ya
haraka kuepuka janga lingine kama hilo.
Meli pamoja na helikopta
za Italia na Malta ziliendelea na shughuli ya kusaka miili usiku kucha.
Mamlaka za Sicily zinasema wengi wa abiria kwenye boti iliyozama
walikuwa ni kutoka mataifa ya Algeria, Misri Somalia, Senegal na hata
Zambia.
Blogger Comment
Facebook Comment